kisa cha mama chakudo na chakudo.

Chakudo alikuwa ni mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi (XXX) huko temeke (2019), alikuwa anaishi na mama yake tu baada ya kuwa wametelekezwa na baba chakudo kwa muda ambapo walikuwa wakiishi katika kata ya azimio, mama chakudo anafanya biashara ya kuuza maandazi na vitumbua, kutokana na ugumu wa maisha chakudo alilazimika kwenda kuuza vitumbua na maandazi kabla ya kwenda shule ili aweze kupata pesa ya matumizi kitu ambacho kilipelekea chakudo kuchelewa shule mara kwa mara na kushuka kitaaluma. baada ya kupita mihula miwili shule na maendeleo yake katika masomo kuendelea kuzorota Zaidi chakudo hakuwezakuendelea na shule hivyo alilazimika kurudi nyumbani na kuendelea kumsaidia mama yake kazi zake za kuuza vitumbua na maandazi. Kila siku asubuhi chakudo alikua akichukua deli la maandazi na vitumbua na kusambaza maeneo mbalimbali.

Siku moja chakudo baada ya kumaliza shughuli yake ya kusambaza vitumbua na maandazi, njiani kuelekea nyumbani alikutana na kundi la Vijana watatu wakamzunguka na kumkaba na kupora pesa zote ambazo alizipata katika biashara yake kwa siku hiyo. Chakudo alifika nyumbani akiwa Analia huku akiwa na majeraha kadhaa katika mwili wake, mama yake alishtuka sana kumuona chakudo na akamfata na kumuuliza “umepatwa na nini”, chakudo akamwambia mama yake kuwa “nimekabwa na wahuni na wakaniibia pesa zote”, mama yake baada ya kusikia hivyo alimkamata chakudo na kuanza kumpiga huku akimshushia kauli za hovyo  kama “muongo wewe,,, huo ni uzembe umefanya,,, nishakwambia uache michezo yako ya ajabu,,, ona sasa umepoteza hela zote mimi nafanyaje, sasa-ondoka hapa ukatafute hiyo pesa mpaka uipate ndipo urudi hapa”, Chakudo aliondoka kwao akiwa mpweke na mwenye huzuni kwa kuwa alikuwa hana mahali pa kwenda, hajui wapi atapata hela ili airejeshe kwa mama yake na wapi atapata chakula kwa ajili ya yeye kuweza kula. Chakudo aliendelea kutembea pasina matumaini yoyote mpaka alipokutana na rafiki yake wa utotoni aitwae Pizo, Pizo alikua ni mtoto mkorofi na mtukutu kitu ambacho kilifanya aache shule mapema akiwa darasa la tatu na pia kufukuzwa na walezi wake nyumbani kutokana na tabia yake ya wizi iliyokithiri kitendo ambacho kilimfanya Pizo awe ni mtoto wa mtaani na awe anajihusisha na wizi na uporaji. Chakudo alimuelezea Pizo mkasa mzima ambao alikutana nao na kumuomba msaada amsaidie kupata chakula na amsaidie kupata mahali pa kulala. Pizo akamwambia chakudo aondoe shaka na asiwe na wasiwasi atamsaidia na huo ndio ukawa mwanzo wa tabia za chakudo kubadilika na kujiunga na vikundi vya wahuni ambao wanajihusissha na wizi na uporaji.

Chakudo alianza kuvuta bangi na kutumia mihadarati, akawa mwizi wakawa wanawapora watu mali zao hadi wakawa wanavamia nyumba za watu na kupora mali zao mara nyingine hata kuwatishia maisha yao kuwa watawaua endapo hawatatoa vitu wanavyo vihitaji.

Mama alisikia wanajamii wakimsema mwanae kuwa amekuwa mwizi mashuhuri katika mtaa wao akaanza kufanya juhudi za kumtafuta mwanae ili aweze kuongea nae pasina mafanikio yoyote.

Siku moja wakiwa katika shughuli zao Chakudo, Pizo na wenzao wawili  waliingia nyumba ya mama mmoja na kuiba pochi ambayo ilikuwa na simu na elfu sitini taslimu (kwa maelezo ya mama aliyeibiwa), yule mama alianza kupiga kelele huku akisema “wezi, wezi, wezi…”, kwa bahati nzuri Pizo na wenzake wawili walifanikiwa kukimbia lakini chakudo pekee ndiye alikuwa na bahati mbaya siku hiyo alikamatwa na wananchi wenye hasira kali na kupigwa mpaka kufa, Na huo ndio ulikua mwisho wa maisha ya chakudo, mama yake alihuzunika sana alipopata habari kuwa mwanae amepigwa mpaka kuuawa, mama chakudo alitamani hata chakudo aamke japo kwa dakika moja ili amuombe msamaha mwanae na kumueleza jinsi gani anajutia kumfukuza mwanae nyumbani lakini hakupata hiyo nafasi kwani chakudo alikua ameshafariki.

Baada ya tukio hilo Pizo ambaye ndiye alimshawishi  chakudo kuingia katika shughuli hizo alijutia na kujilaumu sana kisha Pizo akaelekea kwa mama chakudo na kumsimulia kila kitu jinsi alivyokutana na chakudo na jinsi walivyo ishi, historia ambayo ilimfanya mama chakudo kujutia na kujilaumu Zaidi, kisha Pizo akaahidi kuacha wizi na uporaji kwa ajili ya rafiki yake chakudo.

Mama chakudo alivyopata nafasi ya kuzungumza na maafisa wa Ekama development foundation akaona lazima asimulie mkasa huu uliomkuta ili ukawafikie wazazi wengine katika jamii ili wapate kujifunza na wasiweze kurudia kosa kama alilolifanya yeye.